Nani angethubutu kuhoji uadilifu wa Mungu? Nani angethubutu kupendekeza kwamba Mungu hawezi kuaminika?Walakini, hadithi ya Biblia ya historia ya mwanadamu huanza na madai haya ya kushangaza.
Aliyeibua mashtaka haya hakuwa adui wa Mungu tangu mwanzo. Taswira yake ya kwanza kwenye Biblia inaonyesha akiwa ameheshimiwa sana, akisimama mbele ya Baba yetu wa mbinguni. Kama msemaji wa Mungu aliyeaminika, alitembea kati ya malaika wenzake akibeba nuru na ukweli. Aliitwa “mbebaji wa nuru” – jina ambalo wakati mwingine hutafsiriwa kama “Lusifa” au “Nyota ya Asubuhi” – jina ambalo pia ni la Mwana wa Mungu mwenyewe (ona Ezekieli 28: 1; Isaya 14:12; 2 Petro 1:19; Ufunuo 22: 6).
Lakini Yesu baadaye alimwita “mwongo na baba wa uongo”(Yohana 8:44).Kitabu cha mwisho cha Biblia kinamtaja kuwa “yule nyoka wa kale, aitwaye Ibilisi na Shetani, mdanganyifu wa ulimwengu wote” ( Ufunuo 12:9 ).
“Hakika hamtakufa,” yule nyoka akamwambia Hawa. “Mungu anajua kwamba mara tu mtakapokula matunda ya mti huo, mtafumbuliwa macho, nanyi mtakuwa kama mungu, mkijua mema na mabaya (Mwanzo 3: 4,5, NEB, pembeni). “Mungu haheshimu uhuru na adhama yenu mkiwa watu wenye akili,” Shetani aliendelea kubishana. “Katika jeuri ya ubinafsi anawanyima maarifa na uzoefu ambao ni haki yenu. Amedanganya, na hastahili kuaminiwa.”
Kwa uwongo kama huo, Shetani alikwisha waongoza theluthi moja ya malaika kuwa upande wake dhidi ya Mungu. Ingawa yeye ni kiumbe aliyeumbwa, alikuja kujifikiria yeye mwenyewe kama kimungu. Alisema “Nitapaa juu mbinguni; juu kuliko nyota za Mungu, nitaweka kiti changu cha enzi juu, …Nitapaa juu ya urefu wa mawingu, nitajifanya kama Aliye Juu”(Isaya 14:13,14). Baadaye kiburi cha wendawazimu kilimwongoza hata kumwuliza Yesu, Muumba wake, amwinamie na kumwabudu (Mathayo 4:8-10).
Ili kujiweka mwenyewe kama Mungu kwanza alidhoofisha kuaminika kwa Yule ambaye alitaka kuchukua nafasi yake, na alijaribu kufanya hivyo kwa kuharibu sifa ya Mungu. Kwa kuwa hakuweza kupata kosa lolote kwa Mungu, ilimlazimisha kutumia udanganyifu.
Hivyo ndivyo mapambano ya muda mrefu kwa ajili ya uamainfu wa viumbe vya Mungu huru na wenye akili yalivyoanza. Nani alikuwa sahihi—Mungu au mbebaji wa Nuru iliyometemeta? Inaweza kuwa kweli kwamba Mungu alikuwa holela na pia mkali, asiyestahili upendo na uaminifu wa viumbe alivyoviumba? Ni Mungu wa aina gani angeruhusu tabia yake kupingwa hivyo? Ni nguvu au udhaifu uliompelekea Mungu kuruhusu mjadala mrefu kama huo, na kuruhusu ubishani huu kuenea ulimwenguni?
Mwishowe, Shetani na wafuasi wake walijitosa kwenye uasi wa wazi. Ndipo Mungu, katika mpango wake wa kuona mbali kwa faida ya wote wanaohusika, aliwafukuza waasi kutoka kwa uwepo wake, na ubishi mkubwa ukaenea kwa sayarii hii ambayo tunaishi.
Kama ilivyoelezwa katika lugha ya mfano ya mara kwa mara ya Kitabu cha Ufunuo, “Basi, vita vikazuka mbinguni. Mikaeli na malaika zake wakapigana vita na yule joka.Yule joka na malaika zake walipigana, lakini hawakuwa na nguvu ya kushinda, wala mahali pao hapakuonekana mbinguni. Basi yule joka mkubwa akatupwa chini, yule nyoka wa zamani aliyeupotosha ulimwengu wote, ambaye jina lake ni Shetani, au Ibilisi—akatupwa chini duniani, na malaika zake pamoja naye…..Lakini ole wenu, nchi na bahari, kwa maana yule Ibilisi ameshuka kwenu mwenye ghadhabu nyingi, akijua ya kuwa ana wakati mchache!” (Ufunuo 12:7-9, 12 , NEB).
Siku moja hivi karibuni, kabla Kristo hajarudi, Shetani atafanya jaribio la mwisho kabisa la kutushawishi sote kujiunga na upande wake. Atatokea kama malaika wa nuru—Mbebaji wa Nuru tena; Lusifa; Nyota ya Asubuhi (angalia 2 Wakorintho 11:14). Atajitangaza kuwa ndiye Mungu. Kama vile alivyojaribu kumshawishi Kristo amwabudu katika jangwa la majaribu, ndivyo atakavyo jaribu kutushawishi tumuabudu sasa.
Biblia inatabiri kwamba juhudi za Shetani zitaonekana kufanikiwa kabisa. Ulimwengu wote utamwabudu yeye— isipokuwa wachache, “masalio” (KJV), ambao hawatadanganywa. Badala yake, watachukua msimamo wao na malaika waaminifu na kudumisha imani yao kwa Mungu (ona Ufunuo 12:17; 13:1-8; 14:12).
Sote tumehusishwa bila nafasi ya kuepuka katika pambano hili na matokeoyake. Katika historia yote Shetani amekuwa na mafanikio makubwa katika kupotosha mawazo ya mwanadamu juu ya Mungu. Mamilioni wameabudu miungu ambao hutumia hofu na nguvu kulazimisha mbinu zao. Hata kati ya wale wanaojiita wafuasi wa Kristo, unyanyasaji wa kinyama umekuwa ukifanywa kwa jina la Mungu, wanaume na wanawake waliteswa na kuchomwa moto wakilazimishwa kukubali imani potofu ya Kikristo.
Mara nyingi dini limetaka kukatiza uhuru wanadamu na kuwanyima haki ya utu waliopewa na Mungu! Mara nyingi dini imedhalilisha utu wa binadamu, ikidai washirika wakiri Imani bila kujua ukweli wa Biblia kuhusu mafundisho wanayohitajika kusadiki!
Haya yote yanaashiria kuwa Mungu ni holela na mwenye kiburi. Huu ndio ukweli ambao Yesu alisema utawaweka watu huru? Au huu ni uwongo wa Shetani juu ya Mungu wetu mwenye neema? Mungu anatamani utii unaotokana na uwoga au utii unaotokana na uaminifu na kupendezwa na haki ya njia zake?
Si ajabu kwamba, kwa watu wengi, Mungu amekufa. Mungu ambaye wengine wamemwabudu pengine ni heri akiwa amekufa. Lakini katika utupu unaosalia, je upotovu mbaya zaidi kuhusu Mungu utakusanyika na kuchukua nafasi yake? Hata hivyo binadam hakuumbwa aishi peke yake, bila marafiki, na bila Mungu.
Una picha gani ya Mungu mawazoni mwako? Hiyo picha ni ya kweli? Imekuweka huru? Una marafiki ambao wanafurahia ukweli huo, na ukweli huo umewafanya kuwa watu unaoweza kuwaamini?
Biblia inaelezea umoja maalum ambao upo kati ya wale wanaomjua na kumwabudu Mungu—wanaomwamini na kumpenda jinsi alivyo. Ni furaha iliyoje, pia usalama, na amani ipatikanayo kati ya marafiki wa kuaminika na waaminifu!
Sitasahau kamwe madaktari na timu yao ambao walifanya kazi kwa bidii kumsaidia binti yetu mkubwa wakati alikuwa akiugua ugonjwa mbaya mara kwa mara. Kwa miezi miwili yakwanza wangeweza tu kutoa tumaini lililozuiliwa. Lakini haikuwalazimu kutuambia kuwa walikuwa wakifanya kila kitu ambacho wangeweza kukifanya. Kwa kweli, walitenda, na tulifurahi kwamba walijua ya kwamba tulikuwa tunajua hiyo.
Kwa miaka mingi tuliwajua kama wataalam wazuri zaidi katika fani zao na marafiki wa kuaminika. Wote walimwamini Mungu na waliongea wazi wazi juu ya imani yao. Tulikuwa tumekutana mara nyingi kwa mazungumzo juu ya Mungu, na ujasiri wetu kwake pamoja ulileta hakikisho kubwa wakati huo wa dhiki. Kama ingelikuwa ya kwamba binti yetu hakupona, bado tungejua kwamba marafiki wetu walikuwa wamefanya kila kitu wangeweza.
Mara nyingi nawaza juu ya baba yangu na jinsi alivyotusaidia sisi watoto wake wakati wowote mmoja wetu alipohitaji msaada. Nilijua maisha yangu na sifa zangu zilikuwa salama mkononi mwake. Hata baada ya kuwa watu wazima na kwenda njia zetu tofauti, alikuwa tayari kwenda hadi mwisho wa dunia kutusaidia katika dharura yoyote. Mama vile vile alitujali sana. Hivyo nasema, wazazi wakuaminika hufanya iwe rahisi kwa watoto wao kujifunza kumtegemea Mungu.
Kando na hayo, baba yangu alikuwa ameandika zaidi ya vitabu mia haswa kusaidia watoto, na watu wazima, kuona jinsi Mungu anastahili imani yetu, na sote tulikuwa tukisoma vitabu hivi. Sasa tunawasomea watoto wetu na wajukuu pia hivyo vitabu tukiwa na matumaini kwamba wao pia watachagua wenyewe kumtumaini Mungu. Kwa maana lazima pia tuwape uhuru wao, ikiwa tunawaambia ukweli juu ya Mungu. Ingawa uaminifu ambao Mungu anaotamani lazima uthibitishwe na kila mmoja kibinafsi, nashukuru nakuthamini sana jinsi tulivyosaidiwa na wazazi wetu waaminifu.
Lakini vipi kwa mtu ambaye kwake neno baba sio ishara ya uaminifu? Kasisi wa Jela ya Kaunti ya Erie, New York, alisimulia kwa kufafanua jinsi alivyopata ugumu akijaribu kumhakikishia kijana mmoja juu ya Upendo wa Mungu kwa kusema,”Mungu ni kama baba.” Kijana huyo alijibu “Ikiwa yeye ni kama baba yangu, nina hakika nitamchukia. “
Halafu kulikuwa na msichana mdogo, Aliyeachwa na wazazi kwenye mitaa ya jiji kubwa akiwa na umri wa miaka minane tu. Alimuuliza kasisi, ” Ikiwa Mungu ananipenda kama wewe unavyosema ananipenda, kwa nini aliwaruhusu Mama na Baba waniache?”
Kasisi Burke alijitahidi kupata kitu fulani katika maisha ya watoto hawa wa jiji, ambacho kingeweza kuwa mfano wa kile alitaka kuwaambia juu ya Mungu. Aliwauliza baadhi yao wamsaidie kutafsiri sehemu za Biblia kwa maneno ambayo wangeweza kuelewa.
Mvulana mdogo, ambaye alikuwa anahisi kuwa hakuna mtu ulimwenguni aliyevutiwa kumjali ijapo alionekana kutamani kumpata mtu ambaye angeweza kumwamini, alimsaidia kasisi kutafsiri Zaburi 23. Alifananisha Upendo wa Mungu na mtu mmoja tu ambaye alionekana kumjali, huyu alikuwa afisa wake wa majaribio ya kurekebisha tabia, na kijana huyo alivutiwa naye sana. Hivyo, “Bwana ndiye mchungaji wangu” ikawa “Bwana ni kama afisa wangu wa majaribio ya kurekebisha tabia.”
Mungu ndiye baba yetu sisi sote, na machoni pake sisi sote tu sawa na ni washiriki wa familia yake moja kubwa. Lakini anawezaje kuzungumza na watoto wake, awashawishi vipi waamini, ilhali wanamfikiria Baba kama mlevi asiye na malengo na Mama kama yule kiruka njia?
Anawezaje kuhifadhi imani ya watoto wake Wayahudi ambao walifundishwa kuamini kuwa hawana haja ya kuogopa, kwani Mungu alikuwa pamoja nao? Walikariri ahadi kama vile “Mimi, Bwana Mungu wako, nitakushika mkono wako wa kulia; Mimi ndimi ninayekuambia, “Usiogope, nitakusaidia” (Isaya 41:13). Kisha, nchini ambamo Luther alikuwa amehubiri, waliona mamilioni ya watu wao wakifa na kusikia majirani zao wakiwasaliti kwa maadui zao.
Mungu anawezaje kuhifadhi imani ya watu wapole wa Kambodia waliokimbilia barabarani kuwakaribisha wakombozi wakikomunisti, lakini wakajikuta wakichapwa, kupigwa risasi, na mamilioni kuvurugwa kutoka makwao? Katika kipindi kisichozidi miaka miwili, takriban watu milioni mbili wa Kambodia walifariki. Kijana mkimbizi aliripotiwa akisema “Hakuna upendo mahali popote,” (ona Murder of a Gentle Land, condensed in the Reader’s Digest, 1977). Watu waliandaa uhasama na ukatili huu hawakuficha dharau lao juu ya kumwamini Mungu. Ni vipi watu wa nchi hiyo iliyoharibiwa wataweza kumwamini Mungu na wenzao tena?
Kama Biblia inavyoelezea mwanzo wetu, dunia hii ilikusudiwa kuwa mahali pa uhuru kamili na usalama. Tukiaminiana na kumwanini Mungu, kungekuwa na hofu yanini? Lakini adui wa Mungu ni adui yetu pia. Yule ambaye ametudanganya tusimwamini Mungu anafanya kazi pia kuharibu uaminifu na kuaminika kati yetu na wenzetu. Na ambapo hakuna kuaminiana na kupendana, hakuna uhuru wa kweli wala usalama wa kweli.
Walakini haya ndio mambo ambayo sisi sote tunatamani sana maishani. Tunajihisi vizuri kama wakati wa dharura tunaonyesha kuwa tunaweza kuendelea kuwa marafiki! Tunafurahi sana wakati nchi mbali mbali zinashirikiana kukimbiza dawa na vyakula kwa majirani waliopigwa na majanga ya asili! Ulimwengu wote unapiga makofi wakati meli ya taifa moja inapoingia kuokoa jingine, haswa inapopeperusha bendera ya waliokuwa adui zamani. Hivi ndivyo ulimwengu ulivyohamasika kutazama wakati usio wa kawaida wa kushirikiana kwa umoja, viongozi wa Mataifa walisimama pamoja kwa heshima na huzuni kwenye kaburi la John F. Kennedy (aliye kuwa rais wa 35 nchi ya America).
Ikiwa tu uaminifu wa ulimwengu wote unaweza kurudishwa kwa njia fulani, basi tungweza kufurahia tena uhakika unaoambatana na imani kwa Mungu na kutumainiana. Kisha tunaweza kuhisi kwa mara nyingine tena ile hali ya maana ya adhama na kujistahi inayoletwa na kujua kwamba Mungu na rafiki zetu wanaweza kuweka tumaini lao kwetu kwa usalama.
Lakini tumepoteza sana uwezo wetu na nia ya kuamini. Mbali na hilo, hatari ya kuamini wakati mwingine inaonekana kuwa kubwa sana. Mara nyingi tumekatishana tamaa. Na kwa kukosa kutumainiana, tunaweza kuanza kujiuliza ikiwa ni salama hata kumtumaini Mungu.
Kweli Mungu anaweza kuaminika? Madai tu hayawezi kutatua swali hili. Ibilisi ametoa madai mengi kwa mamlaka na nguvu ya kuvutia. Kinachohitajika ni ukweli, ukweli juu ya Mungu. Kwa vile hatuwezi, kuthubutu, kumwamini mtu ambaye hatumjui.
Lakini Mungu anaweza kujulikana vizuri? Yeye asiye na mwisho amejifunua kwa njia ambayo tunaweza kuelewa na kuwa na hakika kwamba hii ni ukweli? Je, yale tunayoyaona na kuyasikia juu yake (Mungu) yanaongeza uzito huo wa ushahidi kwamba tunaweza kusema, “Hakika mnaweza kumwamini Mungu”?
Biblia inaashiria siku ijayo, ya amani kote ulimwenguni, siku ambayo upendo na uaminifu vitajaza ulimwengu wote wa Mungu. Wakati huo “Wala hawatamfundisha kila mtu jirani yake, na kila mtu ndugu yake, wakisema, Mjue Bwana; kwa maana watanijua wote, tangu mtu aliye mdogo miongoni mwao hadi aliye mkubwa miongoni mwao, asema Bwana’” (Yeremia 31:34).
Wakati huu bado haujafika. Bado kuna ndugu na majirani wengi ambao hawamjui Mungu jinsi alivyo. Wakiwa hawana maarifa au wamepofushwa na uwongo wa Shetani, je wanawezaje kuamua juu ya Mungu? Na wanawezaje kustahimili juhudi za mwisho za Ibilisi kuudanganya ulimwenguni wote?
Hivyo si ajabu kusikia Bwana wetu akielezea kwamba Injili lazima iende ulimwenguni kote kabla ya mwisho kuja (Mathayo 24:14). Mungu asingeuliza mtu yeyote kukabili nyakati ngumu za mwisho zenye shida isioweza kuelezewa, bila nafasi ya kujiandaa (Danieli 12: 1-3).
Nikiwa mvulana wa shule siku zote niliona kuwa jambo la heshima wakati mwalimu wangu aliniuliza nimpelekee taarifa maalum. Heshima na upendeleo viliongezeka kulingana na umuhimu wa ujumbe nilioubeba. Vivyo hivyo, ni fursa yenye heshima ya juu zaidi kwa wale ambao tayari wameamua kumtumaini Mungu kueneza Habari Njema, ukweli ule wa milele juu ya Mungu wetu mwenye neema na kuaminika.
